JINSI JEZI NAMBA 25 INAVYOITESA YANGA

11:46 PM

Namba hii imeonekana kuwa ni chungu kwa timu hiyo, hasa baada ya Oktoba Mosi kunyang'anywa tonge mdomoni na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya watani wao wa jadi Simba kwenye Uwanja wa Taifa.

Mchezaji aliyevaa jezi namba 25, Shiza Kichuya alipiga kona iliyokwenda moja kwa moja hadi wavuni na kuzima ndoto za wanachama na mashabiki hao kuondoka uwanjani na ushindi.

Ilikuwa imesalia dakika tatu kabla ya mechi kumalizika, Yanga ikiongoza kwa bao 1-0, pia ikicheza na wapinzani wao waliokuwa pungufu mchezaji mmoja baada ya Jonas Mkude kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya.

Kichuya amerithi vema namba hiyo ya jezi kutoka mchezaji Emmanuel Okwi ambaye kwa sasa anaichezea Sonderjyske ya Denmark.

Okwi ndiye mchezaji ambaye alikuwa akiisumbua Yanga, licha ya kufunga mabao, lakini alikuwa msaada mkubwa kwa klabu ya Simba hasa kwenye mechi hizo za watani.

Mchezaji huyo hupendelea kuvaa namba hiyo, ikiwa ni mwaka ambao alizaliwa.

Okwi alizaliwa Uganda Desemba 25, 1992. Kutokana na kuwa mchezaji wa mfano na wa kuigwa kwenye klabu hiyo, wachezaji wengi wanaochezea nafasi za mbele wa Simba wanapojiunga kwenye klabu hiyo, kupewa heshima ya namba hiyo au wenyewe kuiomba ili waonekana kufanana na mchezaji huyo aliyepachikwa jina la utani 'Mfalme wa Simba'.

Yanga inavyoteseka na jezi namba 25 dhidi ya Simba

1. Emmanuel Okwi (2012)

Jezi namba 25 ikiwa imevaliwa na Okwi, ilianza kufanya kazi yake Mei 6, 2012 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Aliwavuruga kabisa mabeki wa Yanga na kusababisha kipigo kikubwa cha kwanza kutokea kwenye karne ya 21.

Ilikuwa ni Jumapili mbaya kuwahi kutokea, kwani dakika ya kwanza tu, Okwi alifunga bao.

Mchezaji huyo alikuwa kama 'nyoka' anayeteleza, kwani kasi yake ilisababisha mabeki wa Yanga kumchezea madhambi mara tatu ndani ya eneo la hatari na kusababisha idadi kama hiyo ya penalti.

Zote zilitinga wavuni, zikifungwa na Felix Sunzu dakika ya 58, Juma Kaseja 67 na marehemu Patrick Mafisango dakika ya 72.

Okwi mwenyewe alitumbukiza wavuni bao lingine dakika ya 61, na kuifanya Simba kutoa kipigo cha mabao 5-0.

2. Emmanuel Okwi (2015)

Pia jezi namba 25 ilihusika. Ilikuwa Jumapili nyingine ya Machi 8, 2015, mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/15.

Ilivaliwa pia na Okwi. Ilikuwa mechi ngumu ikiwa moja kati ya mechi chache za hivi karibuni kuchezeshwa vizuri na waamuzi.

Okwi alifunga bao pekee kwenye dakika ya 51 kutokana na ujanja na juhudi zake binafsi, baada ya kuukokota mpira uliookolewa na mabeki wa Simba.

Akiwa pembeni kidogo mwa uwanja, akishambulia kuelekea kusini, aligundua kuwa kipa Ally Mustapha 'Barthez' alikuwa ametoka kidogo, hivyo alipiga shuti la umbali mrefu lililompita kichwani golikipa huyo na kujaa wavuni, Simba ikishinda bao 1-0.

3. Shiza Kichuya (2016)

Akiwa na jezi yake namba 25, Kichuya alimsababishia tena Barthez ashike kichwa. Ikumbuke kipa huyo alilaumiwa sana kwenye mechi aliyofungwa na Okwi.

Oktoba Mosi, Kichuya alimuingiza tena matatani baada ya kupiga kona iliyokwenda moja kwa moja hadi nyavuni.

Kipa, mabeki, wachezaji, benchi la ufundi, wanachama na mashabiki wote wa Yanga hawakuamini kilichotokea.

Bao hilo lilikuja kwa kushtukiza mno na pia wengi waliliona kama la ajabu, hasa ikizingatiwa kizazi cha sasa kwa muda mrefu hakijawahi kushuhudia mabao ya aina hiyo.

Baada ya mechi hiyo, baadhi ya Yanga walionekana kumlaumu kipa wao kuwa hakuwa makini langoni.

Jezi namba 25, ikaendelea kuwatesa tena, kwani mechi hiyo ikaisha kwa sare ya bao 1-1, huku mazingira ya mechi yenyewe yakionyesha kuwa Simba ilikuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

Share this

SPORT HITS IS A BLOG BASED ON PROVIDING SPORT NEWS FROM ALL AROUND THE WORLD, STAY WITH US ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.. Dont Forget to follow us on Facebook, twitter and Instagram @sporthitstz

Related Posts

Previous
Next Post »