TATHMINI YA MCHEZO KATI YA YANGA SC NA AZAM FC

8:58 PM
Na Samuel Samuel 

Mchezo kati ya Azam FC na Yanga SC hapa uwanja wa Amani umemalizika kwa Azam FC kuibuka na ushindi wa goli 4-0 . 

Magoli ya Azam FC yamefungwa na John Bocco , Yahya Mohamedi , Mahundi na Enock Aggyei. 

Ni matokeo ambayo hayakutarajiwa na wengi kutokana na rekodi za timu zote mbili kwenye michuano hiyo . Kabla ya mchezo wa leo Azam ilianza kwa ushindi mwembamba wa goli 1-0 dhidi ya Zimamoto na mechi ya pili kutoka suluhu ya 0-0 na Jamhuri. 

Yanga SC waliochezea kichapo cha 4-0 leo dhidi ya Azam FC, walianza michuano hii kwa kutoa onyo kali baada ya kuichapa 6-0 Jamhuri kisha 2-0 dhidi ya Zimamoto. 

Hapa utaona Yanga wameingia uwanjani leo wakiwa na mtaji mzuri kisaikolojia dhidi ya Azam FC . Yanga wameingia kama tishio mbele ya Azam lakini kibao kimegeuka nakuwaacha watu wengi kinywa wazi . Huo ndio mchezo wa soka na maajabu yake . 

Kimbinu na kiufundi 

Ni msifu sana kaimu kocha mkuu wa Azam FC Idd Nassoro Cheche . Mechi hii imemtambulisha vyema katika uga wa soka nchini na pengine Afrika mashariki yote kutokana na coverage ya runinga ya Azam Media. 

Ushindi huu umejengeka kimbinu zaidi hali inayomfanya kila mdau wa soka kutaka kumjua mwalimu huyu . Licha ya ukongwe wake katika soka lakini si wengi walikuwa wanamfahamu . Amedumu kwenye viunga vya Chamazi Complex kwa miaka mingi akisimama kama kocha wa timu ya vijana ya Azam kazi kubwa kusaka na kulinda vipaji . 

Cheche amekabidhiwa Azam FC baada ya benchi zima la ufundi la timu hiyo kuvunjiwa mkataba takribani wiki mbili zilizopita timu ikijiandaa na michuano hii. 

Mechi mbili za awali dhidi ya Zimamoto na Jamhuri, utaona Azam FC walikuwa wazuri kwenye ulinzi na kiungo lakini wakikosa maelewano mazuri kwenye safu ya ushambuliaji. Ni kawaida sana kimbinu na kiufundi kwa timu iliyobadirisha mwalimu . Mwalimu yoyote yule kwanza ni lazima ahakikishe timu ina ulinzi mzuri na uwezo wa kumiliki mpira kisha ndio huja mbele kwenye kufunga . 

Cheche alimjua vyema Lwandamina katika mechi mbili walizocheza . Alimfahamu na falsafa yake ya kushambulia kwa kasi pande zote lakini muhimili ukiwa kati kwa kutumia viungo wengi .

Cheche amewaingiza uwanjani Azam FC kwa 4-4-2 kama wapinzani wao Yanga walivyoingia lakini akaja kumzidi kete Lwandamina kwenye safu ya kiungo. 

Cheche ampe kongole kiungo wake Abubakar Salumu sanjari na pacha wake Frank Domayo . Hawa ndio waliyoiangamiza Yanga leo. 

Majukumu ya Domayo yalikuwa kukata mawasiliano ya Justin Zullu na viungo wa mbele. Ni kazi rahisi sana kwa kiungo huyu anapokuwa kwenye ubora wake. 

Lwandamina licha ya kumpanga Zullu kama kiungo mkabaji, kiungo huyu alijikua anapwaya vilivyo kutokana na mfumo mzima wa timu ya Yanga SC kiulinzi kuharibika hali iliyomfanya Domayo kupata kazi rahisi kuwatawanya Yanga kati na kutengeneza muunganiko mzuri na Abubakar Salumu aliyekuwa na kazi moja tu kuhakikisha John Bocco na Yahya Mohamedi wanacheza vyema kule mbele. 

Kukosa mawasiliano mazuri kati ya Vicent Andrew na Kelvin Yondani kumlifanya Zullu kushuka chini na kutengeneza uwazi mkubwa mbele yake nafasi ambayo Domayo na Sure boy walikuwa wanaingia na kuwakata Yanga kwenye mipango yao kwenda mbele pia kupanga mashambulizi makali kwenda mbele. 

Kumpanga Mahadhi kama pacha wa Tambwe akitakiwa kuwa na uwezo mkubwa kumiliki mpira , kushuka chini kuchukua mipira kwa viungo wa kati kupeleka mbele pia kujiweka sawa kwenye mashambulizi ya kushitukiza kama striker namba mbili, hapa ndipo alipoanza kuchemka Lwandamina na kuwarahisishia kazi Azam FC . Kiasilia Mahadhi ni kiungo mchezeshaji pembeni au acheze nane " huru " . Hii nayo ilipelekea mipira kushindwa kukaa mbele na kuzidi kumpa kazi nzito Zullu huku Domayo na Sure boy wakiendelea kutawala dimba . 

Lwandamina aliamua kumtoa Mahadhi na kumuingiza Emanuel Martin acheze 11 na Haruna aendelee kucheza huru lakini bado tatizo lilibaki pale pale kwa kiungo cha Yanga chini kuzidiwa . Kipindi cha pili kocha alimtoa Zullu na kumwingiza Saidi Makapu timu ikiwa nyuma 2-0 . Sub haikuwa na msaada zaidi ya kuendelea kupwaya na kuruhusu goli mbili za haraka haraka .

Nini kiliwasibu Yanga leo ?! 

Kwanza kabisa game approach ya mwalimu dhidi ya Azam FC haikuwa nzuri . 

Azam ni timu nzuri na ina wachezaji wazoefu sana wenye anticipation nzuri nje ya mafunzo ya mwalimu . Vipaji binafsi pia kwa sehemu kubwa ni wachezaji ambao wamekaa pamoja kwa muda mrefu chini ya nahodha wao John Bocco . Hii inawafanya kuelewana vyema kimbinu pia kujijenga katika saikolojia ya Ushindi .

Lwandamina alitakiwa aingie vitani kamili sio kujaribu . Licha ya majeruhi ya Ngoma ambaye ndie playmaker namba moja wa Yanga juu akiwa na uwezo wa kutengeneza kombinesheni na viungo takribani wote pale juu ; GL hakutakiwa kumwazisha Mahadhi kama mbadala wa Ngoma au pacha kwa Tambwe .  GL angempanga namba 10 Thabani Kamusoko ambaye ana uwezo mzuri na nafasi hiyo na amewahi kuifanyia kazi mara nyingi tu chini ya Hans Van Pluijm . Kamusoko ana uwezo wa kukaa na mpira , kukaba , kutoa pasi pia kufunga ( qualities of second striker) 

Kamusoko angesimama na Tambwe kushoto Emanuel Martin na kulia Msuva nyuma chini Justin Zullu . Hii wangeweza kutengeneza pressure ya mashambuli mazuri kwa Azam . 

Tazama Full backs Za Yanga leo zilivyokuwa zikikabika kirahisi pale wanapo panda juu kusaidia mashambulizi hiyo ni kutokana na kiungo kushindwa kutanuka kutoa back kwenye holes zilizokuwa zikijitengeneza . 

Ni sawa kumjenga Mwashuiya kama kiraka lakini ni vyema kuangalia zaidi asili yake . Ni rahisi sana kumgeuza Haji Mwinyi kama kiungo mkabaji kuliko Mwashuiya kusimama kama beki . Sidhani kama ana skills zozote za kukaba . Ni vyema aendelee kujengwa kama winga 

Ni kweli mwalimu ni mgeni na anatafuta kikosi bora kwa ajili ya klabu bingwa Afrika mwezi ujao lakini mechi hizi zina heshima zake na rekodi zikiwa mbaya ni ngumu kuzivuta hivyo inampasa kuwa makini . 

Ni mwalimu mzuri na hii ni mechi yake ya kwanza wana Yanga hawana sababu ya kumlaumu zaidi kuzidisha umoja  lakini pia imempa somo kubwa kimbinu na kiufundi hususani kwenye selection ya wachezaji.

Share this

SPORT HITS IS A BLOG BASED ON PROVIDING SPORT NEWS FROM ALL AROUND THE WORLD, STAY WITH US ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.. Dont Forget to follow us on Facebook, twitter and Instagram @sporthitstz

Related Posts

Previous
Next Post »