Miongoni mwa Timu zilizokuwa hazipewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri pengine hata kushika nafasi za katikati isingewezekana basi ni Mbao fc, ambao mpaka sasa wapo katika nafasi ya 9 na pointi zao 13, wakicheza michezo 11, wakishinda 3, droo 4, na kufungwa michezo 4, wkiwa na magoli 13 ya kufunga huku wakiruhusu idadi kama hiyo (13) ya magoli ya kufungwa.
Ni dhahiri Mbao iliyotabiriwa mabaya kutokana na maandalizi duni na kupata nafasi ya ngekewa ya kucheza ligi kuu imeonyesha upinzani na ukomavu wa hali ya juu kiasi cha kuitoa jasho timu ya Simba katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru na Simba kushinda kwa tabu kwa goli 1-0.
Wana mchezo wa nidhamu ya hali ya juu huku wakitambua aina ya mpinzani wanaecheza nae, hawa vijana haswa ni wabishi lakini je! watauweza mziki wa Yanga?
Yanga imetoka kujikusanyia magoli 10 ndani ya mechi 2, ikianza kumfunga Kagera magoli 6-2 kisha kumchapa JKT Ruvu magoli 4-0, safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao watetezi inaonekana kuwa na makali ambayo mpaka sasa imeshapachika magoli 24 wavuni na kufungwa magoli 5 tu huku ikijikita nafasi ya pili na pointi zake 24 wakiifukuzia kwa karibu timu ya Simba iliyojikusanyia pointi 32 ikicheza mchezo mmoja mbele.
Bila shaka utakuwa ni mpambano wa kukatana shoka huku Mbao wakitaka kupata walau pointi moja kutoka kwa mabingwa hao watetezi huku Yanga nao wakitaka kupunguza pengo la pointi waliloachwa na wapinzani wao wakuu Simba sc.
Mtanange huo utapigwa baadae kidogo mnamo saa kumi jioni katika dimba la Uhuru jijini Dsm.

EmoticonEmoticon