Na Ahmada Mwariko
Waswahili wanasema mchelea mwana kulia hulia mwenyewe.. Maneno haya yalisemwa na wahenga na yana busara kubwa sana ndani yake.
Bila shaka hakuna anaeibisha Azam Fc ni miongoni mwa timu bora kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati tena bado wanaendelea kushikilia ubingwa wa Ukanda huu kwa ngazi ya klabu.
Ni klabu pekee iliyowekeza vyema katika miondombinu ya soka na mazingira bora ya kisoka yanayostahili.
Ligi kuu ya Tanzania bara iliendelea jana na kutimiza mzunguko wake wa 7 ambapo timu mbalimbali zilishuka dimbani huku Azam ikiikaribisha Ruvu Shooting star katika dimba la Chamazi na mchezo huo kuishia kwa sare ya magoli 2-2.
Awali kabla ya mechi ya Jana Azam walitoka kupoteza michezo miwili dhidi ya ule wa Simba waliofungwa goli 1 na ule dhidi ya Ndanda uliomalizika kwa Azam kukubali kipigo cha magoli 2-1.
Mpaka sasa Azam imeshapoteza pointi 10 katika michezo saba iliyocheza ikiwa imejikusanyia pointi 11 kati ya 21 na ikiwa katika nafasi ya tano na wikiendi ijayo inaelekea Shinyanga kukipiga na Stand United ambao wanaonekana kuwa moto wa kuotea mbali ma mpaka sasa wanashika nafasi ya pili nyuma ya Simba na pointi zao 15.
Katika michezo yao waliocheza Azam wanaonekana kushindwa kabisa kupambana hasa katika nafasi ya ulinzi na kiungo, kwani katika mpira ilinzi unaanzia kwenye kiungo, mara zote viungo huwa msaada mkubwa kwa walinzi na hata washambuliaji na ndio maana wakaitwa viungo.
Ubinafsi na kutokuwa na mfumo sahihi wa uchezaji kunachangia timu hiyo kufanya vibaya, ukiiangalia michezo ya Azam utakosa jibu kujua Timu hiyo inacheza mfumo gani uwanjani, kila mchezaji anacheza kwa vile uwezo wake unapofikia, Timu imekosa muunganiko, beki zinakatika ni dhahiri mapengo ya kapombe kwa mechi ya jana na Wawa kwa msimu tangia uanze yanajionyesha dhahiri.
Kocha wa Azam mpaka sasa anaonekana kujaribu timu na hana kikosi cha kwanza kitu kinachoonekana ni hatari kiufundi kwa timu kufanya vizuri.
Makosa yaleyale yaliyofanywa na mabeki katika mechi mbili walizopoteza ndio hayohayo yaliyojirudia kwenye mechi ya jana wakati Azam inapambana na Ruvu shooting, hili eneo halijatulia na kuonekana kukosa suluhisho.
Muendelezo wa kubadili makocha nalo huenda ikawa sababu inayoigharimu timu hii, kwani kila kocha ana falsafa zake na tayari kwa msimu ilopita Azam ilionekana tishio chini ya Stewart Hall lakini kocha huyo aliondoka na kukabidhiwa muhispania Hernandez ambae bado mpaka leo hajapata muarobaini wa kikosi hicho.
Nafasi ya ushambuliaji imeonekana kuwa nzito na isiyokuwa na malengo sahihi, katika mechi ya jana dhidi ya Ruvu shooting safu ya ushambuliaji inayoongozwa na John Bocco imeonekana kukosa umakini na kukosa magoli mengi ya wazi.
Endapo Azam watashindwa kutibu ugonjwa wao mapema basi msimu huu utakuwa si mzuri kwao na watajikuta wakilia kilio cha mtu mzima baada ya kuchelea kufanya marekebisho mapema.

EmoticonEmoticon