BAADA ya Simba kufungwa mechi mbili mfululizo huku kipa wao, Vincent Angban akilaumiwa na baadhi ya vigogo wa timu hiyo kuwa anaruhusu mabao laini, sasa miamba hiyo ya Msimbazi imeanza harakati za kunasa saini ya kipa Abbas Pira, aliyewahi kufanya majaribio katika klabu kadhaa, ikiwamo Chelsea ya England.
Simba wanatarajia kufanya usajili wa kipa huyo katika dirisha dogo litakalofunguliwa Novemba 15, mwaka huu, baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, kupendekeza kumleta kipa mwenye uwezo mkubwa ambaye atampa changamoto Angban.
Pira, ambaye ni Mtanzania wa pili kucheza katika klabu ya Chelsea, yeye pamoja na Adam Nditi amekulia katika kituo cha kukuzia vijana cha North Ontony, ambapo alicheza pamoja na mlinzi mahiri wa kati wa klabu ya Manchester United, Chris Smalling.
Kipa huyo amesema yupo tayari kutua katika Mitaa ya Kariakoo ikiwa miamba hiyo ya Msimbazi itatoa dau la Sh milioni 100 ili atue kwenye kikosi hicho aweze kuongeza wasifu wake.
Pira alisema aliwahi kufanya mazungumzo na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Dewji, ambaye alivutiwa na uwezo wake na kuhitaji aende kufanya majaribio katika klabu ya Simba ili ajiunge nao.
Alisema kuwa, kuna klabu mbalimbali zimeonyesha nia ya kumhitaji, siyo Simba pekee, kwani alipata nafasi ya kwenda kucheza ligi kuu ya Kenya, ambapo moja kati ya timu zinazoshiriki ligi kuu nchini humo ilionyesha kutaka kumsajili, lakini walishindwa kufikia makubaliano mara baada ya timu hiyo kushindwa kufikia dau alilotaka.
Alisema iwapo vijana hao Msimbazi watachelewa, huenda akaelekea nchini Ubelgiji, kwani wakala wake anaendelea kumtafutia timu nchini humo.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, anatarajiwa kuchukua uamuzi magumu kwa kuwatema baadhi ya wachezaji nyota na kusajili wapya katika usajili wa dirisha dogo unaotarajiwa kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Omog anatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi baada ya kushindwa kufikia malengo yake ya kushinda kila mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba, pamoja na kuongoza ligi hiyo kutokana na pointi pointi 35, lakini rekodi yake imetibuka baada ya kupoteza mechi mbili za mwisho dhidi ya African Lyon na Tanzania Prisons.
Wekundu hao wa Msimbazi walikuwa hawajafungwa hadi mzunguko wa 13 zaidi ya kupata sare mbili kutoka kwa JKT Ruvu na Yanga, lakini walifungwa bao 1-0 na Lyon, kisha mabao 2-1 na Prisons.
Kutokana na matokeo hayo, Omog amepanga kufanyia kazi upungufu uliojitokeza kwa kuanza kupiga panga baadhi ya wachezaji ambao hawaendi na kasi yake
EmoticonEmoticon