Akiongea na waandishi wa habari msemaji wa Simba Haji Manara amesema kwamba Simba imemuandikia barua Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye kumuomba awaombee msamaha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli waruhusiwe kuendendelea kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Manara alisema kwamba wameona umuhimu wa kuomba radhi kwa kitendo cha mashabiki wachache kuharibu raslimali ambazo zimejengwa kwa kodi za Watanzania wote.
“Rais ndiye msimamizi wa raslimali za nchi hii, hivyo tumemuandikia barua Waziri Nape kumuomba atuombee radhi kwa Rais Magufuli, kwa kitendo cha mashabiki wetu kung’oa vitu kwenye mchezo wa Oktoba 1 (2016) dhidi ya Yanga”, alisema Manara.
“Wakati tukiwa jukwaa kuu na kuona tukio lile likitendeka, tulitamani kuruka kwenda kuwazuia mashabiki wasing’oe viti, lakini hatukuweza, ilikuwa mbali, lakini tunaaahidi tukio kama lile halitatokea tena, kwani limeshusha thamani ya klabu yetu,”alisema.
Aidha, Manara ameiomba Serikali kupitia Menejimenti ya Uwanja wa Taifa kufunga kamera ili kunasa matukio kwa lengo la kuwabaini wahusika wa uharibifu. Akawaomba pia askari Polisi wanaopangiwa kusimamia usalama uwanjani kuhakikisha wanawatazama mashabiki badala ya kuangalia mchezo ili kujiweka tayari kupambana na wahalifu.

EmoticonEmoticon