WASANII BONGO WAAMUA KUREJESHA ENZI ZA TAMTHILIA, HIZI NI TATU KUTOKA KWA RAY, J B NA JOHARI NA IRENE UWOYA

12:41 AM
Tamthilia za kwenye runinga zimetengeneza mzizi wa filamu za Tanzania. Kwa lugha nyingine, kama kusingekuwepo na maigizo ya kwenye TV, pengine kusingezaliwa mastaa wengi wa filamu tulionao sasa. Karibu asilimia 80 ya waigizaji wa filamu wanaofanya vizuri hapa kwetu wametokea kwenye vikundi vya maigizo vilivyokuwa vikirusha vipindi vya kwenye TV, hususan, ITV enzi hizo.

Mastaa kama marehemu Steven Kanumba, Ray Kigosi, JB, Johari, Elizabeth ‘Lulu’ Michael, Single ‘Rich’ Mtambalike’, Monalisa, Mzee Chilo, Bi. Hindu, Cloud, Dr Cheni na wengine, walianza kujipatia umaarufu kwenye tamthilia. Vikundi kama Kaole Sanaa Group, Kidedea, Mambo Hayo na vingine vilichangia kwa kiasi kikubwa kukomaza vipaji vya uigizaji walivyokuwa navyo wasanii wengi.

Enzi hizo malipo waliyokuwa wanapata wasanii kupitia tamthilia zao yalikuwa duni na hayakuweza kuwafaidisha kwa lolote. Wengi walifanya kwa passion na wale waliostahimili walikuja kuanza kula matunda baada ya soko la filamu za Tanzania kuchipuka. Miaka michache baada ya filamu kuanza kuonekana zinalipa, wasanii wengi walijitoa kushiriki kwenye tamthilia na kuingia kwenye filamu.

Tamthilia za kueleweka zikapotea kabisa kwenye TV na kubaki maigizo ambayo hayajawahi kuzalisha mastaa tena na hakuna mtu anayeyachukulia serious kama zamani. Hiyo ndiyo miaka ambayo marehemu Kanumba na wenzake walianza kuvuma kwenye filamu. Filamu za Tanzania zikapendwa kiasi cha kuzitoa kabisa sokoni filamu za Kinaijeria ambazo miaka ya 1995s zilikuwa zimetokea kupendwa.

Waigizaji wakaanza kupata fedha kupitia filamu na wengi walifanikiwa kuanzisha makampuni yao. Tasnia ya filamu ilikuja kupata pigo mwaka 2012 baada ya kifo cha Kanumba aliyekuwa amezifikisha filamu za Tanzania mbali kiasi cha kuanza kula sahani moja na mastaa wa Nollywood.

Pamoja na waigizaji kama JB, Ray na wengine wapya walioibuka kama Irene Uwoya, Irene Paul, Rose Ndauka, Wema Sepetu, Shamsa Ford, Hemedy, Jacqueline Wolper na wengine wa miaka hii kama Gabo, Rammy Galis na wengine (kwa uchache tu) kuja na filamu nzuri, kifo cha Kanumba kilisababisha pengo kubwa. Leo hii wasanii wengi wanalalamika kuwa soko la filamu kudoda kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu mbalimbali.

Habari njema ni kwamba wasanii taratibu wanaanza tena kurudi kwenye thamthilia. Ni jambo la kufurahia kwasababu kiukweli hata Marekani kwa miaka mingi sana series za kwenye TV zimegeuka kuwa na soko kubwa. Vituo vya runinga vinashindana kutayarisha series za kuvutia na hivyo kuwapa waigizaji wengi zaidi ujira kuliko kutegemea tu filamu. Series nzuri huvutia udhamini wa makampuni makubwa na hivyo kuwaingizia mkwanja mzuri waigizaji na watayarishaji.

Ongezeko la uhitaji wa vipindi kwenye TV za Tanzania limewafanya sasa waigizaji wa filamu kuanza kufikiria kurudi tena kwenye thamthilia. Hizi ni tamthilia mpya zitakazokuja soon kwenye TV yako:

Kiu ya Kisasi – Jacob ‘JB’ Stephen



JB ni muigizaji bora kabisa wa filamu wa kiume Tanzania kwa sasa. Amefanikiwa kuigiza filamu kali zilizofanya vizuri sokoni. Ni muigizaji mwenye kipaji halisi, anayebeba uhusika na mwenye uwezo wa kucheza aina nyingi za filamu zikiwemo za komedi. Kupitia kampuni yake ya Jerusalem Films, JB kwa miezi kibao sasa amekuwa location kutayarisha series yake iitwayo Kiu ya Kisasi.

Ninaamini hii itakuwa series ya kuotea mbali na itakayotambulisha pia vipaji vipya vya uigizaji kwasababu anadai asilimia 80 ya waigizaji wa tamthilia hiyo ni wapya. Bado hajasema ni kituo gani cha runinga kitairusha lakini anadai TV kibao zimetoa offer.

Drama Queen – Irene Uwoya



Drama Queen ni jina sahihi kwa wajihi wa Irene Uwoya. Filamu zote nilizowahi kuziona za muigizaji huyu nilizipenda sana. Uwoya ana kipaji kikubwa na utampenda akibeba uhusika wa msichana jeuri. Ninaamini jina tu la series hii linasadifu makavu na maisha ya kutoyumbushwa ya mhusika mkuu wa series hii ambaye ni yeye mwenyewe. Irene alitueleza kuwa tamthilia zimeanza kulipa tena na vituo vingi sasa hivi viko interested.

Ray na Johari, RJ Company



Ray na Johari bado hawajataja jina la tamthilia yao lakini walisema tayari kampuni yao, RJ Company imeanza kutayarisha tamthilia yao pia. Wawili hawa ni nguli kwenye tamthilia na miongoni mwa mastaa waliozaliwa kupitia kundi la Kaole.

Nachukua fursa hii pia kuwapongeza Clouds TV kwa tamthilia yao ya vijana ya Kelele na EATV kwa tamthilia yao ya Siri za Familia. Ninaamini miaka michache ijayo ushindani kwenye tamthilia nzuri za Kiswahili utarejea kwa kasi zaidi.

Share this

SPORT HITS IS A BLOG BASED ON PROVIDING SPORT NEWS FROM ALL AROUND THE WORLD, STAY WITH US ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.. Dont Forget to follow us on Facebook, twitter and Instagram @sporthitstz

Related Posts

Previous
Next Post »