RAIS MAGUFULI| TUMESIMAMISHA AJIRA NA KUPANDISHA VYEO ILI KUHAKIKI

12:10 AM
Rais John Magufuli amesema Serikali imeamua kusimamisha ajira mpya kwa muda usiozidi miezi miwili pamoja na upandishaji wa vyeo kwa watumishi wa umma kwa lengo la kupisha uhakiki wa wafanyakazi katika orodha ya malipo ya mshahara na kuondoa watumishi hewa.

Akizungumza jana katika Jubilei ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kazi hiyo haina nia ya kuwakatisha tamaa watumishi wa umma, bali Serikali itaendelea kuajiri baada ya kukamilika kwake.

“Serikali ninayoiongoza haina nia ya kuwakatisha tamaa wafanyakazi. Lengo lake ni kujipanga kwa makosa tuliyoyafanya na ndiyo maana nimesema kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi au hata mwezi mmoja na nusu, haitazidi miezi miwili, tusiajiri mtumishi yeyote serikalini,” alisema Rais Magufuli.

“Katika kipindi cha mwezi mmoja hatutawapandisha vyeo wafanyakazi. Ninaomba wafanyakazi waelewe hili, kwa sababu tukiendelea tutakuwa tunawapandisha vyeo hata wafanyakazi ambao hawapo. Tunafanya ukaguzi wote tukishamaliza, wafanyakazi wataendelea kupandishwa vyeo.”

Rais Magufuli aliipongeza BoT kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kipindi cha miaka 50 katika kusimamia sekta ya fedha na maendeleo, lakini ameitaka kuchukua hatua za haraka dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoyahusu majukumu yake.

Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni idadi ndogo ya Watanzania wanaonufaika na huduma za benki, hususan waishio vijijini, benki kutoza riba kubwa na hivyo kusababisha wananchi kuogopa kukopa kwa hofu ya kushindwa kulipa.

Nyingine alisema ni kuilinda thamani ya shilingi ya Tanzania na kukusanya kodi ipasavyo kwa miamala inayofanywa kupitia simu za mkononi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Rais Magufuli pia aliagiza BoT kuchukua hatua mara moja dhidi ya benki ambazo hazizalishi faida, kama benki za Serikali, kufuta akaunti zisizo hai na kuanzisha mara moja akaunti moja ya mapato na matumizi ya Serikali.

Share this

SPORT HITS IS A BLOG BASED ON PROVIDING SPORT NEWS FROM ALL AROUND THE WORLD, STAY WITH US ALL THE TIME FOR INSTANT UPDATES.. Dont Forget to follow us on Facebook, twitter and Instagram @sporthitstz

Related Posts

Previous
Next Post »